Magoti na Gyan kulipa fidia ya zaidi ya shilingi milioni 17

0
155

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam imewahukumu Afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti na mwenzake Throdory Gyan ambaye ni mtaalam wa mfumo wa kompyuta, kulipa fidia ya zaidi ya shilingi milioni 17 baada ya kupatikana na hatia ya kuongoza genge la uhalifu.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, – Janeth Mtega baada ya washtakiwa hao kukiri mashtaka yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Mbali na kulipa fidia, mahakama hiyo pia imewahukumu Washtakiwa hao adhabu ya kutokutenda kosa lolote la jinai kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia leo.

Hakimu Mtega amesema, mahakama hiyo imewatia hatiani Washtakiwa hao kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

“Washtakiwa mmetiwa hatiani kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa, hivyo mnatakiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni kumi na saba laki tatu, Hamsini na nne elfu mia tano thelathini na tano (Mill.17, 354,535 ) kama fidia kwa Serikali,” amesema Hakimu Mtega.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, amedai kuwa kesi hiyo ilipelekwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi kutokana na Washtakiwa kukiri mashtaka yao.

Wakili Kadushi amesema Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu, lakini baada ya kufanya majadiliano na DPP, wamefutiwa mawili na kubakisha shtaka moja ambalo ni kuongoza genge la uhalifu.

Aidha Wakili mwandamizi wa Serikali Wankyo Simom amedai kuwa Mshtakiwa Magoti, Gyan na wenzao ambao hawajafikishwa mahakamani, walishiriki makosa ya uhalifu wa kupanga kwa kumiliki programu ya kompyuta iliyotengenezwa mahususi kwa ajili ya kufanya uhalifu na kujipatia fedha kiasi cha shilingi milioni 17, 354,535, kosa ambalo wanadaiwa kulitenda kati ya Februari mosi na Desemba 17 mwaka 2019 katika maneno tofauti jijini Dar es salaam.

Upande wa utetezi ukiongozwa na Fulgence Massawe akisaidiwa na Jebra Kambole na Pasiansi Mlowe, wameomba mahakama hiyo kuwapunguzia adhabu washitakiwa hao kwa madai kuwa ni vijana wadogo na wanategemewa na familia zao na kwamba wameonyesha ushirikiano tangu siku ya kwanza walipofikishwa mahakamani hapo.