Jeshi la polisi mkoani Pwani linamsikilia Baraka Njoka mkazi wa wilaya ya Ubungo mkoani Dar es salaam kwa tuhuma za kusafirisha madumu 860 ya mafuta ya kupikia yanayodaiwa kuingizwa nchini bila kulipiwa ushuru.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Pwani, – Wankyo Nyigesa amesema kuwa, Baraka amekamatwa na askari wa doria katika eneo la Lugoba wilayani Bagamoyo.
Amesema kuwa, mafuta hayo yalikuwa yamepakiwa kwenye lori aina ya Fuso lenye namba za usajili T 582 AWB ambalo lilikua likiendeshwa na Baraka.
Katika tukio jingine Kamanda Nyigesa amesema kuwa, Jeshi la Polisi mkoani Pwani limemkamata Mustafa Malimi ambaye ni mmoja wa Wafungwa walioachiliwa huru kwa msamaha wa Rais John Magufuli tarehe Tisa mwezi huu wakati wa sherehe za miaka 58 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa tuhuma za wizi wa ngómbe.
Amesema kuwa, mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa mfungwa katika gereza la Ubena kabla ya kuachiliwa huru tarehe 10 mwezi huu, amekamatwa katika eneo la Nero Magorofani katika mji wa Chalinze baada ya kuiba na kumchinja ngómbe mwenye thamani ya Shilingi Milioni Moja na Laki Mbili.
Kamanda Nyigesa amesema kuwa, Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.