Madiwani waaswa kuipa kipaumbele ajenda ya miundombinu ya michezo

0
148

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amewataka madiwani kuipa kipaumbele zaidi ajenda ya ujenzi na uboreshaji wa miundo mbinu ya viwanja vya michezo katika halimashauri zao, akisistiza kuwa michezo ni kipaumbele kikubwa kwa jamii, kama ilivyo kwa vipaumbele vingine.

Waziri Bashunwa ametoa wito huo wakati akizungumza katika fainali ya ligi ya Mtaturu Cup iliyofanyika viwanja vya shule ya Sekondari Ikungi mkoani Singida.

Amesema Serikali inatamani kuboresha viwanja vyote vya michezo ili viwe na viwango vinavyostahili lakini wakati mchakato ukiendelea ndani ya Serikali ni vyema madiwani kupitia vikao vyao vya  halimashauri wakaipa kipaumbele ajenda ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya viwanja vya michezo katika maeneo yao.

Kuhusu uelewa mdogo wa sheria za mchezo wa Soka, Waziri Bashungwa amewaahidi wakazi wa Ikungi kuwa,  atawaagiza wataalam kutoka Chuo cha Michezo cha Malya kufika wilayani Ikungi kwa ajili ya kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yanayo tawala mchezo huo.

Awali akizungumza katika kilele cha Mtaturu Cup mwandaaji wa ligi hiyo ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu amesema dhamira kuu ya mashindano hayo imefikiwa kwa kiwango kikubwa, na kuhahidi kuwa ligi hiyo itakuwa endelevu kwa lengo la kujenga mshikamano zaidi kwa vijana.

Katika fainali hizo timu ya Matongo imebuka mabingwa kwa kuichapa bao mbili kwa nunge timu ya Mampando na kujizolea zawadi ya kombe pamoja na fedha taslimu shilingi milioni 1.5.