Madini kuchangia 10% pato la Taifa 2025

0
120

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa yote nchini kuhakikisha wanatunza takwimu za madini ya aina zote yanayozalishwa nchini katika kanzidata.

Pia amewataka kuendelea kusimamia vema sekta ya madini ili mchango wake kwenye pato la Taifa uendelee kukua na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
 

Waziri Biteko ametoa agizo hilo mkoani Dodoma kwenye kikao chake na menejimenti ya Tume ya Madini.

Amesema Serikali kupitia wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha mchango wa sekta hiyo kwenye pato la Taifa unafikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 na kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli lililowekwa na Serikali kwa mwaka 2022/2023 la shilingi bilioni 822.

Waziri huyo wa Madini amesisitiza kuwa wizara hiyo itaendelea kuipa ushirikiano Tume ya Madini ili iweze kufikia malengo yake ikiwa ni pamoja na kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya madini.