Serikali imesema itapeleka watumishi wa afya 112 katika hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini Mtwara ili kuhakikisha hospitali hiyo inahimili idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma katika hospitali hiyo.
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya Godwin Mollel wakati akijibu swali la mbunge Abdallah Chikota wa jimbo la Nanyamba aliyetaka kujua ni lini serikali itapeleka watumishi wa kutosha katika hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini Mtwara.
Amesema hospitali hiyo ilizinduliwa mwezi Oktoba mwaka 2021 ikiwa na watumishi 45 na ili kuhakikisha wananchi wananufaika na hospitali hiyo, kwenye kibali cha sasa cha ajira serikali imewapanga watumishi 112 na itafanya idadi ya watumishi kuwa 157 watakaoweza kuleta matokeo chanya ya uwekezaji uliowekwa katika hospitali hiyo.
Aidha Naibu Waziri Mollel amesema hospitali hiyo ina madaktari bingwa wawili tu na kwa kibali cha sasa wamepeleka madaktari bingwa 8 na hivyo hospitali hiyo itakuwa na madaktari bingwa 10.
Hata hivyo Naibu Waziri Mollel amesema vifaa tiba vya kuimarisha utendaji katika hospitali hiyo vimeagizwa nje ya nchi na hadi mwezi Oktoba mwaka huu hospitali hiyo itakuwa imeshapata vifaa hivyo.