MADAI YA WAITARA NA MULUGO YACHUNGUZWE

0
122

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson ameitaka serikali ifanye uchunguzi ndani ya kipindi cha miezi mitatu ili kupata uhalisia wa malalamiko ya Wabunge Mwita Waitara wa jimbo la Tarime Vijijini mkoani Mara na Philipo Mulugo wa jimbo la Songwe, ambao wamedai bungeni kwamba baadhi ya wananchi wa majimbo yao wameuawa na tembo na wengine kupigwa risasi na kunyanyaswa na askari wa wanyamapori.

Dkt. Tulia ametoa maelekezo hayo leo bungeni jijini Dodima baada ya kusoma ushahidi uliowasilishwa kwake na Wabunge hao baada ya kuwataka wafanye hivyo.

Baada ya kusoma ushahidi huo Spika Tulia amesema ushahidi wa Wabunge hao wawili haujitoshelezi na kwa kuwa wabunge sio vyombo vya uchunguzi ni lazima serikali ifanye uchunguzi utakaowasilishwa bungeni.

Wakati wakichangia bajeti ya wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 mbunge Mwita Waitara na Philipo Mulugo walidai kuwa baadhi ya wananchi katika majimbo yao wameuawa na tembo na wengine wamepata ulemavu na wengine wamekuwa wakinyanyaswa na askari wa wanyamapori, jambo lililomlazimu Spika kuwataka wapeleke ushahidi bungeni.

Aidha Spika Tulia amewataka Wabunge wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa taarifa zenye ushahidi ndani ya bunge, kwani wao ndio wawakilishi wa wananchi na kwamba bunge haliwezi kupewa taarifa za mauaji ya wananchi na kukaa kimya.