Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni, amewaeleza wananchi wa Kijiji cha Nanguruwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, kuwa hadi ifikapo mwezi Machi 2024, vitambulisho vya Nida vitapatikana nchi nzima.
Akijibu moja ya kero na changamoto za wananchi zilizowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, Shamsia Mtamba, wakati wa Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani Mtwara, Masauni amesema kuwa hadi sasa vitambulisho milioni 2 tayari vimepokelewa.
Ameongeza kuwa kwa wakati huu, namba za utambulisho zinaendelea kutumiwa kutoa huduma zote na kuwataka wananchi kutambua kuwa kutopata vitambulisho hakutawazuia kupata huduma.
Aidha, ameziagiza taasisi za umma nchini zinazotoa huduma kwa wananchi kutokumnyima mwananchi huduma kwa makosa yasiyo yake.