Maboresho ya vipindi TBC yamkuna Waziri Bashungwa

0
189

Serikali imelipongeza Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutokana maboresho makubwa iliyofanya kwenye vipindi vyake mbalimbali na kuahidi kuendelea kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa shirika hilo.

Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa wakati wa ziara yake katika ofisi za TBC jijini Dar es salaam.

Amesema maboresho makubwa yaliyofanywa na TBC katika vipindi vyake mbalimbali, yamesababisha vipindi hivyo kuwa na wapenzi wengi ndani na nje ya nchi.

“Kwa kweli TBC inatazamwa na watu wengi, mfano wa wazi ni Rais wa Uganda Yoweri Museveni, mara kadhaa amekuwa akiisifia TBC, hii inaonesha kupendwa kwake ndani na nje ya nchi,” amesema Waziri Bashungwa.

Akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt Hassan Abbasi, Viongozi hao wamepata fursa ya kutembelea vitengo mbalimbali vya TBC na kupatiwa maelezo ya utendaji kazi wake.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt Ayub Rioba Chacha amesema shirika hilo litaendelea kuboresha vipindi vyake mbalimbali, pamoja na kuboresha usikivu wa matangazo yake.

“Pamoja na kufanya vizuri kwa kipindi hiki, lakini bado tuna changamoto, na kubwa ni kutokuwa na bajeti ya kutosha ya maendeleo,” ameongeza Dkt Rioba.

Shirika la Utangazaji Tanzania linamiliki vituo vitatu vya televisheni na vitatu vya redio.