Mabilioni yatengwa kulipa malimbikizo ya mishahara ya Watumishi

0
1495

Serikali imeahidi kulipa malimbikizo yote ya mishahara ya Watumishi wa Umma, na kwamba tayari shilingi bilioni 20 zimetengwa kulipa madai ya Watumishi ambao maombi yao yamekwishaidhinishwa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi Rasilimali Watu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ibrahim Mahumi wakati akizungumza katika Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) jijini Dar es salaam.

Kuhusu kuchelewa kulipwa kwa malimbikizo hayo, amesema kumetokana na Mfumo wa Rasilimali Watu (LAWSON) kulemewa na madai ya Watumishi yaliyoanza kupokelewa kwa wingi kufuatia Serikali kukamilisha zoezi la kuhakiki taarifa za watumishi (kuondoa watumishi hewa na wasiokuwa na elimu stahiki kulingana na ngazi zao).

Pia amesema baadhi ya Watumishi hawajalipwa malimbikizo yao kwa sababu maombi yao hayajapokelewa, lakini ameahidi kuwa wote wenye madai halali watalipwa kwani tayari Serikali imeanza kutumia mfumo mpya wa kushughulikia malimbikizo.

Mahumi ametumia jukwaa hilo kuwakumbusha Watumishi wa umma kuzingatia maadili sehemu za kazi ikiwa ni pamoja na kufahamu nani anatakiwa kutoa taarifa fulani kutokana na kuzuka kwa tabia ambayo kila mmoja anataka kuwa msemaji wa shirika au taasisi.

Ameongeza kuwa mitandao ya kijamii imechangia kumomonyoka kwa maadili kwa sababu wapo Watumishi wasio waaminifu wanaovujisha taarifa za siri za Serikali mitandaoni.