Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mafia mkoani Pwani, – Erick Mapunda kuyavunja Mabaraza yote ya ardhi ya Kata na Vijiji yasiyotenda haki wakati wa kutoa maamuzi katika wilaya hiyo.
Dkt Mabula ametoa agizo hilo akiwa katika ziara yake ya siku Mbili wilayani Mafia, kwa lengo la kuhamasisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na kukagua masijala ya ardhi.
Amesema kuwa, kutokana na kero nyingi za ardhi alizozipokea katika ziara yake wilayani Mafia, amebaini Mabaraza ya ardhi ya Kata na Vijiji katika wilaya hiyo hayafanyi kazi zake vizuri na Wajumbe wake wamekuwa wakiyatumia kutoa maamuzi yasiyotenda haki.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, kadri Mabaraza ya ardhi ya Kata na Vijiji katika wilaya ya Mafia yanavyofanya vibaya katika utoaji maamuzi yake, hata uanzishwaji Baraza la Ardhi la Nyumba la wilaya hiyo halitafanya vizuri katika utendaji wake.
“Ukiwa na watu wasioweza kusimamamia haki itakuwa shida sana, Mkurugenzi hakikisha Mabaraza ya Ardhi katika Kata na Vijiji yasiyofuata taratibu na kutoa haki kwa walalamikaji unayavunja na kuteua Wajumbe wapya” amesisitiza Naibu Mabula.
Ametaka kupitiwa upya Mabaraza yote ya ardhi ya Kata na Vijiji katika wilaya ya Mafia hasa yale yanayolalamikiwa na kubainisha kuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi iko tayari kutoa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi ya Nyumba nchini ili atoe elimu katika Mabaraza hayo kwa lengo la kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Baadhi ya Wakazi wa Mafia wamelalamikia Mabaraza ya ardhi ya Kata na Vijiji wilayani Mafia kwa kusema kuwa Wajumbe wake wamekua hawatendi haki wakati wa kutoa maamuzi na hivyo kuonesha dhahiri uwepo dalili za rushwa.
Awali Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya wilaya ya Mafia Erick, – Mapunda alieleza kuwa Mabaraza ya ardhi ya Kata na Vijiji katika wilaya hiyo yapo na yanafanya kazi na wajumbe wake wamewezeshwa kwa kupatiwa mafunzo.