Mabalozi watakiwa kusimamia diplomasia ya uchumi na siasa

0
341
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo kwa watumishi (hawapo pichani) wakati wa mkutano

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa ubalozi pamoja na kukagua mali za serikali nchini humo.

Balozi Ibuge kabla ya kuanza kukagua mali hizo, alikutana na watumishi katika mkutano ambapo amewataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa.

Balozi Ibuge akipatiwa maelekezo kutoka kwa Afisa wa Ubalozi wakati wa ukaguzi wa mali zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania nchini Ethiopia

“Nawasihi sana kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake tufanye kazi kwa bidii na kuwa wabunifu wa kuitangaza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Pamoja na Mambo mengine, Balozi amesihi ubalozi huo kuhakikisha kuwa wanatekeleza vyema vipaombele vya serikali ya awamu ya tano kama ilivyoelekezwa kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020 – 2025) katika sura ya saba, ambapo sura hiyo imeelekeza balozi zote kutekeleza diplomasia ya uchumi pamoja na diplomasia ya siasa.

Kwa upande wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Elizabeth Rwitunga amemhakikishia Balozi Ibuge kuwa watafanya kazi kwa umoja, bidii, weledi na ubunifu kwa maslahi ya Taifa.

Rwitunga ameongeza kuwa mashirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia ni mazuri na yanaendelea kuimarika ikiwemo ushirikiano katika masuala ya usafiri wa anga ambapo Shirika la Ndege la Ethiopia linashirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika masuala mbalimbali ikiwemo mafunzo na matengenezo ya ndege ambapo tayari watanzania watatu (3) wameshapatiwa mafunzo ya ndege.

Aidha, ameahidi kusimamia sera ya diplomasia ya uchumi pamoja na diplomasia ya siasa kwa kuhakikisha wanawasiliana na wawekezaji mbalimbali wa kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za nishati, usafirishaji, utalii pamoja na biashara.

Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia unaiwakilisha Tanzania pia katika nchi za Djibouti, Yemen, Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia masuala ya uchumi barani Afrika (UNECA).