Rais Samia Suluhu Hassan amewapangia vituo vya kazi Mabalozi wakiwemo Mabalozi Wateule sita aliowateua Mei 10, 2023.
Rais Samia pia amewabadilisha vituo vya kazi Mabalozi wanne.
Mabalozi waliopangiwa vituo vya kazi ni pamoja na Balozi Fatma Mohammed Rajab kuwa Balozi wa Tanzania nchini Oman kuchukua nafasi ya Balozi Abdallah Abasi Kilima ambaye amestaafu.
Balozi Joseph Sokoine anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada kuchukua nafasi ya Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ambaye mstaafu.
Balozi Naimi Sweetie Hamza Aziz anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Austria na Meja Jenerali Ramson Mwaisaka (Balozi Mteule) anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Rwanda kuchukua nafasi ya Balozi Meja Jenerali Richard Makanzo ambaye amehamishiwa Cairo, Misri.
Gelasius Byakanwa (Balozi Mteule) anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Burundi na anakwenda kuchukua nafasi ya Balozi Jilly Maleko ambaye amestaafu na
Habibu Awesi Mohamed (Balozi Mteule) anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Qatar kuchukua nafasi ya Balozi Mahadhi Juma Maalim ambaye amehamishiwa Kuala Lumpur, Malaysia.
Wengine ni Imani Njalikai (Balozi Mteule) ambaye anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Algeria akichukua nafasi ya Balozi Meja Jenerali Jacob Kingu ambaye amestaafu, Hassan Iddi Mwamweta (Balozi Mteule) anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani kuchukua nafasi ya Balozi Abdallah Possi ambaye amehamishiwa Geneva, Uswisi na Dkt. Mohamed Juma Abdallah (Balozi Mteule) anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia kuchukua nafasi ya Balozi Ali Jabir Mwadini ambaye amehamishiwa Paris, Ufaransa.
Mabalozi waliohamishwa vituo ni Balozi Ali Jabir Mwadini kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa kuchukua nafasi ya Balozi Dkt. William Shelukindo ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Meja Jenerali Richard Makanzo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri kuchukua nafasi ya Balozi John Nchimbi ambaye anarejea nyumbani, Balozi Abdallah Possi kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa Geneva, Uswisi kuchukua nafasi ya Balozi Maimuna Tarishi ambaye amemaliza mkataba wake na Balozi Dkt.John Simbachawene kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uganda kuchukua nafasi ya Balozi Dkt. Aziz Mlima ambaye amestaafu.
Mabalozi Wateule wataapishwa Agosti 16, 2023 saa 5 asubuhi Ikulu, Chamwino, Dodoma.