Mabalozi waaswa kustawisha uhusiano baina ya Tanzania na Mataifa mengine

0
151

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka mabalozi aliowaapisha leo, Agosti 21, 2021 kuhakikisha wanakwenda kujenga mahusiano mema baina ya Tanzania na mataifa wanayokwenda kufanya kazi.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha mabalozi watatu, Rais Samia amesisitiza mabalozi hao kwenda kutafuta masoko kwaajili ya maslahi ya nchi.

Rais Samia amewataka mabalozi hao kutafuta nafasi za kazi na za uongozi ambazo Watanzania wana uwezo wa kuziomba na kuziongoza ikiwa ni fursa ya mahusiano ya kimataifa yanayoendelea kujengwa hivi sasa.

Kuhusiana na fursa za kiuchumi, Rais Samia Suluhu Hassan amesema mabalozi wote aliowateua wana uwezo mkubwa na ushawishi wa kidiplomasia hivyo wakatumie uzoefu walionao kufungua fursa za kiuchumi hapa nchini.

Akizungumzia utendaji wa mahakama, Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka mtendaji mpya wa mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel kuhakikisha anaongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika shughuli za mahakama na kuboresha utoaji haki kwa kutumia mahakama zinazotembea.

Mbali ya kuwaapisha mabalozi hao Rais amemvisha cheo na kumuapisha Mnadhimu Mkuu wa Jeshi, Luteni Jenerali Mathew Mkingule ambaye anachukua nafasi ya Luteni Jenerali Yakub Mohamed ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uturuki.