Mabadiliko ya kiutendaji yasaidia kuongeza ufanisi

0
150

Serikali ya Awamu ya Tano yafanikiwa kuleta mabadiliko ya kiutendaji yaliyosaidia kuongeza ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza leo jijini Dodoma, kwenye kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binandamu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, George Mkuchika alisema “Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, inasimamia kikamilifu maadili katika utumishi wa umma, na katika kipindi cha miaka minne tumeshuhudia mabadiliko makubwa katika utumishi wa umma.”

Aliongeza “kiwango cha uadilifu katika utumishi wa umma kimeongezeka kwa kiasi kukubwa. Hivyo, ninapenda kutumia nafasi hii kuwapongeza watumishi wote ambao wameitikia wito wa Serikali wa kuzingatia maadili katika utumishi wa umma”

Waziri Mkuchika, alibainisha juhudi mbalimbali ambazo Serikali imezichukua katika kuhakikisha utumishi wa umma unazingatia maadili, ikiwa ni pamoja na kutunga sheria mbalimbali zinazosimamia wa utendaji katika Utumishi wa Umma kama vile Sheria Na. 13 ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Kanuni za Maadili ya Utumishi wa Umma, na miongozo mingine ya kiutumishi ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara.

Adha, jitihada nyingine za Serikali ni maboresho katika programu mbalimbali, pamoja na kuimarisha uadilifu katika sekta ya umma, kwa kutekeleza Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpangokazi wake, ambapo taasisi zote za umma zinapaswa kuwa na Kamati za Kusimamia Uadilifu.

Vilevile, Waziri Mkuchika amewataka viongozi wote katika utumishi wa umma kusimamia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha utumishi wa umma kuwawezesha wananchi kupatiwa huduma bora na bila usumbufu wa aina yoyote.

Ambapo, alisisitiza kuwa  Rais Magufuli, amekuwa kila mara akionesha kutokuvumilia watendaji wabovu  Serikalini, na  wananchi wameonyesha kufurahishwa na juhudi na msimamo wa Rais pamoja na Serikali yake katika kusimamia maadili katika utumishi wa umma. Umakini na uharaka wa Serikali katika kuchukua hatua dhidi wa watumishi wasiozingatia maadili.