Maabara mpya ya kupima madini yazinduliwa Dar

0
2009

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea maelezo kutoka kwa mtaalam wa maabara ya kupima madini iliyozinduliwa leo Ijumaa Dar es salaam

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua maabara ya kisasa yenye uwezo wa kupima na kutambua aina mbalimbali za madini.

Maabara hiyo iliyofunguliwa leo Ijumaa, katika Kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC) kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam, itasaidia kupunguza migogoro ya umiliki wa madini na kudhibiti utoroshwaji wa madini mbalimbali kati ya nchi moja na nyingine.

“Maabara hii litatuweza kulinda madini yetu na kufanya biashara ya madini vizuri. Pia hii ni fursa nzuri kwa nchi za Afrika kutumia maabara hii kupima madini yao na kubaini yalikotoka,” Waziri Mkuu amesema.

Waziri Mkuu pia amewataka viongozi wa kituo hicho kuhakikisha wanaziwesha nchi wanachama kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya madini pindi zinapohitaji.

Ameishukuru Serikali ya Ujerumani kwa kusaidia katika ununuzi wa vifaa vya maabara hiyo pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu watakaoiendesha.Waziri Mkuu, pia ameiomba Serikali hiyo kutoa mafunzo hayo kwa Watanzania wengi zaidi ili kuongeza idadi ya wataalamu wa kuendesha maabara hiyo.

Pia, Waziri Mkuu amefungua Mkutano 38 wa Mawaziri wa Madini kutoka nchi Wanachama wa Ukanda wa Maziwa Makuu unaofanyika katika kituo cha AMGC.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini ikiwa ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama zilizosheheni wanyama wa aina mbalimbali pamoja na fukwe za bahari.