Leseni 2411 za uchimbaji madini zimetolewa Geita

0
108

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema Mkoa huo umetoa leseni 2411 za uchimbaji madini ili kuongeza chachu katika uchimbaji madini na huku kipaumbele chao katika utoaji wa leseni hizo ni wachimbaji wadogo na wanawake.

Shigella ameyasema hayo wakati wa ufungaji wa maonesho ya Sita ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita ambapo amesema bado wanaendelea kutoa leseni za uchimbaji madini na katika leseni hizo zilizotolewa, kuna kundi la wachimbaji wadogo wanawake 300 ambao wamepewa leseni.

Pia Shigella amesema wanaendelea kuandaa maonesho ya madini mkoani humo ili kuongeza juhudi za kuufanya Mkoa huo kuongoza kwa uchangiaji wa mapato Serikalini baada ya mkoa huo kushika nafasi ya 7 katika kuingiza mapato serikalini kwa mikoa yote Tanzania.

Ameongeza kuwa washiriki katika maonesho ya mwaka huu wameongezeka kutoka 250 kwa mwaka 2022 na kufikia 350 kwa mwaka 2023 kutoka mataifa 7 (Mwenyeji Tanzania, Kenya, Malawi, Burundi, China, India na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo).