Kura zaendelea kupigwa Afrika Kusini

0
492

Raia wa Afrika Kusini wanaendelea kupiga kura kumchagua Rais wa nchi hiyo pamoja na Wabunge, huku Chama Tawala cha African National Congress (ANC) kikipewa nafasi kubwa ya kushinda.

ANC inapewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo,  licha ya kuwepo kwa kashfa za rushwa kwenye serikali inayoongozwa na chama hicho, kuyumba kwa uchumi wa Afrika Kusini pamoja na ukosefu wa ajira.

Chama cha ANC ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1994, kimeshinda katika chaguzi zote Tano zilizopita na kinapewa nafasi ya kushinda tena, ingawa sio kwa  kura nyingi.

Habari zaidi kutoka nchini Afrika Kusini zinasema kuwa vyama 47 vya upinzani vinashiriki uchaguzi huo  wa Rais na Wabunge, lakini vyama pekee vikuu vya upinzani vya Democratic Alliance ( DA) na kile cha Economic Freedom Fighters ( EFF), ndivyo vina upinzani mkubwa.

Vituo vya kupigia kura vitafungwa saa tatu usiku kwa saa za Afrika Kusini, lakini kwa wapiga kura watakaokuwa ndani ya vituo kabla ya muda  huo, wataruhusiwa kupiga kura yao.