Kukosekana kwa Uzalendo kwamsikitisha Rais Magufuli

0
212

Rais John Magufuli ameonesha kukerwa na baadhi ya watu waliokosa Uzalendo kwa nchi yao na kufurahia kuzuiliwa kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) nchini Afrika Kusini.

Rais Magufuli amesema kuwa, watu wa aina hiyo inabidi waombewe ili wapate ufahamu na kujitambua kwani ndege hiyo ilinunuliwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akiwahutubia Wanachi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha Pipes Industries kilichopo vingunguti jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa, jitihada za serikali ni kuona nchi inakuwa na uwezo mkubwa wa kumiliki vitu vyake kama ndege, lakini anasikitishwa na baadhi ya watu wanaofurahia mali zao zikishikiliwa ama kuzuiliwa.

“Nawaomba Baba Askofu na Sheikh muwaombee hao watu ili pepo wawatoke, haiwezekani watu wafurahie ndege iliyonunuliwa kwa fedha zao ikishikiwa na watu wengine”, amesema Rais Magufuli.

Ndege ya Tanzania aina ya Airbus 220-300 ilishikiliwa nchini Afrika Kusini kwa muda wa siku Kumi, kwa amri ya mahakama ya Gauteng mjini Johannesburg kabla ya kuachiwa na mahakama hiyo mwanzoni mwa mwezi huu.