Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nenelwa Mwihambi amezitaka Kamati zote za Bunge zilizokuwa zikutane kuanzia tarehe 10 na nyingine kuanzia tarehe 17 mwezi huu zisifanye hivyo, na badala yake zikutane wakati wa mkutano wa Sita wa Bunge unaotarajiwa kuanza Februari Mosi hadi 11 mwaka huu kwa utaratibu na tarehe zitakazotangazwa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mwihambi amesema hatua hiyo inatokana na kuendelea kwa taratibu za uchaguzi wa kujaza nafasi ya Spika wa Bunge hilo baada ya Job Ndugai kujiuzulu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Spika ndiye kiongozi wa Bunge na ndiye msimamizi wa shughuli zote za Bunge, hivyo kiti chake kinapokuwa wazi hakuna shughuli yoyote itakayotekelezwa katika Bunge isipokuwa uchaguzi wa Spika.
Taarifa hiyo ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewataka Wabunge wote kufika Dodoma tarehe 31 mwezi huu.