KUFANYIKA MKUTANO WA SADC HAPA NCHINI NI HESHIMA KWA TANZANIA- WAZIRI JAFFO

0
422

Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Suleiman Jaffo amesema, kufanyika kwa mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika –SADC hapa nchini ni heshima mara mbili kwa Tanzania

Waziri Jaffo amesema heshima ya kwanza ni kwa nchi kuwa mwenyeji wa mkutano huo mkubwa wa kimataifa ambao unatoa fursa kwa watanzania kuonesha utamaduni kwa mataifa mengine 11 ya Kusini mwa Afrika.

Ameongeza kuwa Heshima ya Pili ni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kukabidhiwa kiti cha Uenyekiti wa SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Akizungumza na TBC Online Waziri Jaffo amesema, matukio yote mawili yanaonesha heshima kubwa itakayoipata Tanzania wakati na baada ya mkutano huo.

Aidha waziri Jaffo amewataka watanzania na hasa wanafunzi kufuatilia mijadala itakayokuwa ikiendelea wakati wa Mkutano huo ili kujifunza mambo mbalimbali ya Jumuiya hiyo.

Mwisho amewataka watanzania kudumisha Amani na utulivu ambayo ndio tunu ya utanzania na kuwakarimu wageni wote watakao kuja kwenye mkutano huo wa SADC.