Kiwanda cha TBPL chatakiwa kujitangaza

0
153

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amekitaka kiwanda cha kutengeneza viuadudu (TBPL) kilichopo Kibaha mkoani Pwani kuhakikisha kinajitangaza ndani na nje ya nchi, ili kuongeza wigo wa masoko kwa kuuza bidhaa hiyo ya kipekee.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kushuhudia namna uzalishaji wa dawa za viuadudu unavyofanyika.

Akiwa kiwandani hapo Dkt. Kijaji amekiagiza kuhakikisha kinajitangaza kwa nguvu zote ili kupata masoko ya ndani na nje ya nchi badala ya kutegemea soko la ndani ambalo kwa kiasi kikubwa si la kuridhisha.

Awali akimkaribisha Waziri Kijaji, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambalo ndio mmiliki wa kiwanda hicho Alfred Mapunda amesema, shirika hilo kwa kushirikiana TBPL wameanza utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kimasoko ikiwemo kuhakikisha mkataba wa mauzo baina ya NDC na wizara ya Afya unasainiwa, pamoja na kuanza mchakato wa upatikanaji wa mawakala wa kuuza na kusambaza dawa hizo hapa nchini.