Kiwanda cha Dangote chapanda miti 1,000

0
252

Katika kuzindua maadhimisho ya Wiki ya Utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, wafanyakazi wa kiwanda cha Saruji Dangote mkoani Mtwara leo wameungana na wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Mtwara kupanda miti 1,000 kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza malengo hayo.

Wafanyakazi hao wakiongozwa na Mkurungezi wa Uendeshaji wa Kiwanda cha Dangote, Annadurai Appavoo wamepanda miti hiyo katika eneo la Kiwanda hicho cha Dangote, eneo la hifadhi ya chanzo cha maji katika kijiji cha Mbuo na eneo la Shule ya Msingi ya Dunstan Kyobya iliyopo katika Kijiji cha Hiari.

“Dangote kama Taasisi duniani kote wiki hii ni muhimu sana kwetu, tunaungana na Umoja wa Mataifa kutekeleza malengo endelevu 17 ambapo kitaifa sisi Dangote Tanzania tunatekeleza malengo matatu ambapo moja wapo ni kutatua changmoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi,” amesema meneja mawasiliano wa kiwanda hicho, Rachael Singo.

Singo amesema watanzania wengi wamekuwa na tabia ya kukata miti sababu ambayo imekuwa ikipelekea kuwepo kwa athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambazo huathiri mazingira na maisha ya watu, ikiwa ni pamoja na kukosa hewa safi.

Abdullhali Mohammed, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuo, ameshukuru uongozi wa kiwanda hicho kwa kupanda miti katika kijiji hicho akisema miti hiyo itasaidia katika kulinda mazingira na chanzo cha maji kilichopo katika eneo la kijiji.

“Kwanza ninashukuru Dangote kwa zoezi hili la upandaji miti maeneo ya kijiji changu hii itatusaidia kuhifadhi vyanzo vyetu vya maji ili visiweze kukauka, vyanzo vya maji vikikauka ni hasara kwa jamii nzima, na kwa bahati nzuri vyanzo hivi vinanywesha vijiji visivyopungua 14.”

Aidha, ameuomba uongozi wa Kiwanda hicho kufikiria kupanda miti zaidi huku akiahidi kutunza na kulinda miti hiyo ili ikue kwa faida ya jamii na vizazi vijavyo.