Naibu Spika wa bunge Dkt. Tulia Ackson amesema kuna umuhimu wa serikali kukipandisha hadhi ya kuwa hospitali kamili kituo cha afya Kifula cha wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati akikabidhi gari ya kubeba wagonjwa pamoja na kuzindua wodi za wagonjwa zilizojengwa na mfuko wa maendeleo ya watu wa Ugweno kwa kushirikiana na taasisi ya Tulia Trust.
Majengo hayo yamefanyiwa ukarabati, ujenzi wa wodi mbili, vifaa vya kisasa na gari la kubebea wagonjwa kwa kituo cha afya Kifula kilichopo wilayani Mwanga.
“Kituo hiki ni faraja kwa wakazi wanaoishi katika tarafa ya Ugweno na maeneo ya jirani kwani wataondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya” alisema Naibu Spika Dkt. Tulia.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema kwa sasa watapata huduma ya afya karibu na hivyo kupunguza adha ya kwenda Hospitali ya Usangi kufuata huduma.