Kinyagigi wafurahia mradi wa EACOP

0
106

Wananchi wa kata ya Kinyagigi Singida Vijijini waliopisha mradi wa bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani Tanga wamesema, wapo tayari kuchangamkia fursa mbalimbali kutokana na mradi huo.

Wananchi hao wa vijiji vya Kinyagigi na Mitula katika kata hiyo ambao kwa sasa wanahakikiwa maeneo yao na mali zao wamesema, wanafurahi kupitiwa na mradi huo na wamejiandaa kuchangamkia fursa zitakazojitokeza.

Miongoni mwa wananchi hao wa Kinyagigi ni Ally Mtinangi ambaye amesema kuwa msimamizi wa mradi huo ambaye ni EACOP, mbali na kulipa fidia amekuwa akitoa elimu ya ujasiriamali na kilimo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kinyagigi Musa Esya amesema, hadi sasa hakuna malalamiko yoyote kutoka wa wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

“Tunaendelea vizuri na hakuna malalamiko hata moja hadi sasa, tupo vizuri na kuna waliokuwa wanashindwa kutafsiri lugha ya kiswahili lakini tumesaidia na kila mtu amepata haki zake. Tupo tayari kushirikiana na EACOP mwanzo hadi mwisho kujenga mradi utakaotunufaisha sisi na Watanzania wote.” ameongeza Esya

Msimamizi wa fidia kutoka ofisi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania TPDC, Barnabas Yesaya amesema, wanapata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi na zoezi linaendelea vizuri.

Katika kata ya Kinyagigi, kaya zilizopisha mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki ni 59 kutoka kijiji cha Kinyagigi na 33 kijiji cha Mitula?, ambapo kwa sasa zoezi linaloendelea ni kuhakiki taarifa zao.