Kilio cha Dkt. Tulia kwa Waziri Mkuu

Mbeya, Tanzania

0
144

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Aksion amemueleza Waziri Mkuu kuwa licha ya kufanya vizuri katika makusanyo ya fedha za umma lakini Jiji la Mbeya bado lina hali mbaya ya miundombinu hasa ya barabara.

Akizungumza wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Mpango wa tatu wa utoaji mafunzo wa Uanagezi kwa Vijana hapa nchini, uliofanyika Mkoani Mbeya, Dkt. Tulia amesema, hali ya Barabara katika Jiji la Mbeya ni mbaya na imekuwa ikisababisha ajali za mara kwa mara.

Dkt. Tulia amesema, mbali na ubovu wa Barabara lakini pia Jiji la Mbeya linakabiliwa na uhaba wa Shule na kwamba kata zaidi ya kumi zinategemea shule moja pekee ya sekondari jambo linalokwamisha upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wengi.

Kuhusu huduma za afya, Dkt. Tulia amesema kuwa bado hali ya upatikanaji wa huduma hizo ni duni na kwamba mitaa zaidi ya 110 inategemea vituo chini ya sita vya afya katika jimbo hulo.

Akijibu maombi hayo ya Dkt. Tulia, Waziri Mkuu amesema anatambua tatizo la barabara linawakabili wananchi wa Mbeya na kwamba serikali inafanya jitihada za kuziboresha barabara hizo.

Waziri Mkuu amesema, changamoto zilizotolewa na Naibu Spika zitafanyiwa kazi na kutatuliwa kwa wakati