Waziri wa Maji Jumaa Aweso amewasimamisha kazi watumishi wanne wa wizara hiyo kufuatia kusuasua kwa ujenzi wa bwawa la Kwankambala wilayani Handeni mkoani Tanga.
Waziri Aweso ametangaza uamuzi huo jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na wadau wa sekta ya maji wa wilaya ya Handeni.
Watumishi waliosimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi ni Hamisi Matungulu ambaye ni Msimamizi wa mradi huo kutoka Wakala wa Maji na Usafi wa Mazimgira Vijijini ( RUWASA) makao makuu, Jimmy Mwanyakunga – Mhasibu Mkuu RUWASA
makao makuu, Amos Mtweve ambaye ni Meneja Udhibiti Ubora wa Miradi na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi RUWASA makao makuu na Zam Mlimira – Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi naye kutoka RUWASA makao makuu.
Waziri Aweso amekutana na Wadau hao wa maji wa wilaya ya Handeni na kutangaza uamuzi huo baada ya ziara yake aliyoifanya wilayani humo tarehe 12 mwezi huu ambapo alibaini mkandarasi anayejenga bwawa la Kwankambala amelipwa zaidi ya shilingi milioni 600 sawa na asilimia 33 ya gharama ya mkataba, huku kazi iliyofanyika ikiwa ni asilimia 20.
Aidha, iligundulika kampuni iliyopewa kandarasi ya kazi hiyo iitwayo Civil Loth Enterprises Ltd iliondoa vifaa vya kazi katika eneo la ujenzi, ingawa ilikuwa imeongezewa muda wa utekelezaji wa ujenzi.
Mbali na kuwasimamisha kazi watumishi hao, Waziri Aweso ameagiza kufanyika mapitio ya mkataba wa nyongeza wa mkandarasi na kuundwa tume ya Uchunguzi ili kubaini changamoto zinazokabili utekelezaji wa mradi huo.
Pia ameagiza kushikiliwa kwa mkandarasi Civil Loth Enterprises Ltd kwa hatua za uchunguzi zaidi na ametaka kufanyika kwa taratibu nyingine ili ujenzi wa bwawa hilo la Kwankambala lililopo wilayani Handeni mkoani Tanga uendelea.