Kijana aua watoto wawili, naye auawa

0
453

Watoto wawili wa familia moja wameuawa  kikatili  katika Kitongoji cha Kwazoka wilayani Kibaha mkoani Pwani, baada ya kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Yasin Abdala  kuvamia nyumbani kwao na  kisha kuwakata kwa panga.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa amesema kuwa  tukio hilo limetokea baada ya kijana huyo anayefanya kazi za ndani jirani na eneo hilo  kuvamia nyumbani kwa  mama mzazi wa watoto hao, Saada Maulidi  ambaye pia amejeruhiwa.

Amewataja watoto hao kuwa ni Rehema Makolo mwenye umri wa miaka mitano  na mwanafunzi wa darasa la awali katika shule ya Kwazoka na Abubakari Makolo mwenye umri wa miaka sita na mwanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya msingi kwazoka.

Kamanda Wankyo  amesema kuwa baada ya mauaji hayo baadhi ya majirani walifika nyumbani kwa mwanamke huyo na kumkamata kijana huyo na kwenda kumfungia katika ofisi ya Kijiji  cha Kwazoka.

Amesema akiwa ndani ya ofisi hiyo, kijana huyo alivunja mlango na kukimbia na ndipo wakafanikiwa kumkamata  tena na kumshambuliwa kwa kutumia za zana za  jadi ambapo baadae alifariki dunia.

Mama mzazi wa watoto hao amelazwa katika Kituo cha Afya cha Mlandizi huku hali yake ikielezwa kuwa ni mbaya na miili  ya watoto hao  ikiwa imehifadhiwa katika kituo hicho afya.