Kesi ya Zumaridi yapangiwa hakimu mpya

0
224

Hakimu Monica Ndyekobora ameondolewa kusikiliza shauri la jinai namba 12/2022 linalomkabili Diana Bundala maarufu kama Mfalme Zumaridi na wenzake 83 badala yake shauri hilo litasikilizwa na Hakimu Mkazi, Clescensia Mushi.

Leo Jumatatu Agosti Mosi 2022 kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kusikiliza hoja kutoka kwa mawakili wa utetezi jambo ambalo halikufanikiwa baada ya Hakimu Mkazi, Clescensia Mushi kupanda mahakamani hapo na kutangaza kwamba shauri hilo limepangwa chini yake kuanzia leo huku akiitaarifu mahamakama kwamba atasikiliza shauri hilo kwa siku tatu mfululizo kuanzia Agosti 15 mwaka huu.

Bila kutaja sababu za Ndyekobora kuondolewa, Mushi aliagiza upande wa Jamhuri kupeleka mashahidi watatu siku hiyo ili kuendelea na usikilizaji wa ushahidi baada ya shahidi mmoja kati ya 20 wa Jamhuri kumaliza kutoa ushahidi wake chini ya Hakimu Ndyekobora.