Kesi ya Mbowe yaahirishwa

0
198

Mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Freeman Mbowe na wenzake watatu, wamesomewa upya mashtaka katika kesi ya ugaidi inayowakabili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mkoani Dar es Salaam.

Mshitakiwa Mbowe na wenzake wamesomewa upya mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Thomas Simba, baada kuunganishwa na washitakiwa wenzake katika kesi hiyo ambapo awali walisomewa mashitaka yao wakiwa tofauti.

Hata hivyo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza mashtaka ya ugaidi na kesi za uhujumu uchumi.

Katika kesi ya Msingi Mbowe na wenzake watatu wadaiwa kutenda kosa la kula njama, kutenda makosa ya uhalifu ikiwa ni pamoja na kufadhili ugaidi makosa ambayo wanadaiwa kutenda kati ya Mei Mosi na Agosti Mosi , 2020 katika maeneo tofauti mkoni Dar es Salaam, Morogoro, Moshi na Arusha.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni pamoja na Halfan Hassan,Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenywa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 13 Agosti 2021 baada ya upande wa Jamhuri kudai ofisi ya DPP hijakamilisha taratibu za kuifungua kesi hiyo kwenye mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza.

Emmanuel Samwel TBC