Mahakama ya Wilaya ya Arumeru iliyopo Sekei jijini Arusha ameahirisha kesi ya mauaji inayomkabili Mkami Shirima hadi Aprili 8 mwaka huu itakapotajwa tena baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ombi hilo mahakamani hapo.
Wakili wa Serikali, Amalia Mushi akizungumza mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Abelaide Kasala, amesema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Katika kesi ya msingi, Machi 14 mwaka huu mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa shtaka la mauaji ya mfanyakazi wa ndani Salome Zakaria (18), kosa analotuhumiwa kulitenda Machi 6, 2020.
Aidha, baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, mtuhumiwa alipandishwa tena kizimbani mbele ya Hakimu Gwantwa Mwankuga akikabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kilo 2.9.
Kesi hiyo pia imeahirishwa hadi Aprili 8 mwaka huu.