Kero ya umeme, TANESCO yapewa siku tano

0
214

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametoa muda wa siku tano kwa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuhakikisha linafanya matengenezo ya mtambo wa kufua umeme ili kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara katika baadhi ya maeneo nchini.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameagiza matengenezo ya mitambo mbalimbali ya kufua umeme nchini yakamilike ndani ya siku tano au chini ya hapo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata umeme wa uhakika.

Dkt. Kalemani ametoa agizo hilo mkoani Dar es Salaam baada ya kukagua kituo cha umeme cha Songas ambacho mitambo yake miwili inafanyiwa matengenezo na hivyo kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 115 badala ya 180.

Aidha, kuhusu muda wa kufanya matengenezo ya mitambo ya umeme nchini, Dkt. Kalemani ameiagiza TANESCO na Songas kupishanisha muda wa matengenezo ili kutoathiri hali ya upatikanaji wa umeme nchini.

Vilevile, Dkt.Kalemani amesisitiza kuhusu utekelezaji wa agizo alilolitoa kwa TPDC la kuhakikisha kuwa vifaa mbalimbali vinavyotumika kwenye miundombinu ya gesi nchini kama vile valvu na mabomba vinatengenezwa nchini ili kurahisisha upatikanaji wa vifaa husika.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Songas, Anael Samuel, alimueleza Waziri Kalemani kuwa matengenezo ya mitambo miwili ya umeme kwenye kituo hicho, yanaenda sambamba na matengenezo katika bomba la gesi kutoka Songosongo linalopeleka gesi kwenye mitambo hiyo ya Songas ili kuzalisha umeme.

Amesema kuwa, kutokana na bomba hilo la gesi kutoka Songosongo kufanyiwa matengenezo, kwa sasa megawati 115 zinzozalishwa kwenye kituo hicho zinatokana na mitambo ya gesi ya Shirika la Maendeleo Tanzania (TPDC).

Kwa upande wake Meneja Mitambo wa Songas, Michael Mngodo amesema kituo cha umeme cha Songas kina mashine sita ambapo kwa sasa mashine zinazofanya kazi ni nne na zinazofanyiwa matengenezo ni mbili.

Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Titto Mwinuka amemuhakikishia Dkt Kalemani kuwa watasimamia matengenezo ya mtambo huo na hivyo kumaliza tatizo hilo la kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo nchini.