Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto amemuahidi Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa ana uhakika vikwazo 14 vya kibiashara vilivyobaki kati ya nchi hizo mbili vitatatuliwa kabla ya mwaka huu kuisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam katika siku ya pili ya ziara yake nchini Rais Ruto amesema kuwa, kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia na Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta ya kutatua vikwazo 54 vya kibiashara visivyo wa kikodi vimeinufaisha zaidi Tanzania.
Ahadi hiyo imekuja baada ya Rais Samia kueleza kuwa kati ya vikwazo 68 visivyo vya kikodi vilivyotambuliwa, vikwanzo 54 vimepatiwa ufumbuzi na vikwazo 14 bado havijatatuliwa.
Aidha, Rais Ruto amesema kuwa mradi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Kenya utakuwa ndio mradi wake wa kwanza, na kwamba atahakikisha unakamilika kwa wakati ili wananchi wa Kenya wapate nishati hiyo kwa gharama nafuu.
Viongozi hao wawili wamekubaliana pia kushirikiana katika sekta ya utalii na maliasili huku Rais Ruto akisema kwamba, “kama wanyama wanaweza kufanya mambo yao bila tatizo, basi na sisi tufanye mambo yetu bila tatizo.”