Kenya: Mvua zasababisha vifo vya watu 200

0
196

Mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya Magharibi mwa Kenya zimesababisha vifo vya watu wapatao 200 huku wengine zaidi ya 100,000 wakilazimika kuyahama makazi yao.

Mvua hizo ambazo mwezi Aprili zilinyesha kwa wingi pia zimesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ikiwemo ya barabara .

Katika eneo la Budalangi, Magharibi mwa nchi hiyo nyumba nyingi zimezingirwa na maji baada ya Mto Nzoia kufurika ambapo watu wamekuwa wakitumia boti kuzifikia nyumba zao.

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Kenya imeonya kwamba mvua hizo zitaendelea kunyesha huku zikitarajiwa kupungua mwezi huu.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Fred Matiang’i amesema juhudi za kuwahamisha watu katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko yaliyoambatana na maporomoko ya udongo zinaendelea.

Wakati akisema hilo, Waziri wa Nishati Charles Keter amesema mabwawa mawili makubwa ya kuzalisha umeme ya Masinga na Turkwel yamejaa maji na yameanza kufurika hatua inayotishia usalama wa watu wanaoishi jirani na mabwawa hayo.