KCMC, Mawezi zilivyohusika ubadhirifu milioni 520 za NHIF

0
147

Wizara ya Afya imesema imebaini uwepo wa ubadhrifu wa zaidi ya shilingi milioni 520 katika miamala ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani Kilimanjaro.

Ubadhirifu huo unadaiwa kuhusisha watumishi sita kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda KCMC pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao kazi na viongozi wa mkoa, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema ukaguzi huo maalum unaitaja Hospitali ya KCMC kuongoza kwa ubadhirifu wa shilingi milioni 245 ikifuatiwa na Hospitali ya Saint Joseph, milioni 46, pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi, milioni 38, ambapo watumishi hao wameghushi nyaraka na kujipatia fedha hizo kinyume na sheria.

Dkt. Mollel ameongeza kuwa ubadhirifu huo pia umefanywa na baadhi ya watumishi kwa kushirikiana na baadhi ya maduka ya dawa za binadamu ambapo uchunguzi unaendelea zaidi ili kubaini wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ameviagiza vyombo vya usalama kuwakamata watumishi wote waliohusika kufanya ubadhilifu huo pamoja na kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa.

Sauda Shimbo, Moshi