Kazi ya uokoaji yaelekea ukingoni

0
2182

Mkuu wa majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo amesema wanajitahidi kuhakikisha kazi ya kuwaokoa watu waliozama kufuatia kupinduka kwa kivuko cha MV Nyerere inakamilika hii leo ili kazi ya kuhifadhi miili ianze.

Akizungumza na tbc kutoka katika eneo kilipozama kivuko hicho, Jenerali Mabeyo amesema kuwa kwa wale ambao watakuwa hawajatambuliwa na ndugu zao wataomba kibali cha serikali ili wahifadhiwe karibu na eneo ilipotokea ajali hiyo.

Mapema hii leo, fundi mkuu wa kivuko hicho cha MV Nyerere ameokolewa akiwa hai wakati zoezi la uokoaji likiendelea.

Mhandisi Augustino Charahani ni miongoni mwa wafanyakazi Wanane wa kivuko cha MV Nyerere ambaye alikuwemo ndani ya kivuko wakati ajali hiyo inatokea.

Hadi kufikia mchana wa leo miili ya watu 60 imeopolewa na kufanya idadi ya watu waliokufa kufikia 197.