Kazi ya kusambaza umeme wilayani Chato yaendelea

0
113

Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa maagizo iliyoyatoa kwa Mkandarasi anayefanya kazi ya kusambaza umeme vijijini wilayani Chato mkoani Geita kampuni ya Whitecity Guangdong JV.

Mwenyekiti wa Bodi ya REA, -Julius Kalolo ameyasema hayo wilayani Chato mara baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme inayoendelea wilayani humo.

Amesema kuwa, maagizo ya Bodi ya REA yalitolewa siku 14 zilizopita, ambapo Mkandarasi huyo alielekezwa kutekeleza kazi ambazo alikuwa hajafanya kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo kuchimba mashimo, kusimika nguzo na kuvuta nyaya ili kuweza kuwasha umeme katika vijiji alivyopangiwa ameweza kuyatekeleza.

” Tulitoa maagizo haya wiki mbili zilizopita baada ya kufanya ziara wilayani hapa na kukuta nguzo zimelala na Mkandarasi alikuwa haonyeshi kama alikuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa kasi tunayotaka, lakini baada ya kukagua leo tumeona nguzo zimesimikwa na nyaya zimeanza kuwekwa kwenye nguzo, hivyo ameweza kutekeleza maelekezo”, amesema Kalolo.

Mkandarasi huyo pia ameanza kazi ya  kufunga transfoma kwa ajili ya kusambaza umeme kwa Wananchi, hivyo Bodi hiyo ya Wakala wa Nishati Vijijini imemtaka kuongeza kasi ili maeneo yote muhimu pamoja na Wananchi waunganishiwe umeme.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni  hiyo ya Whitecity Guangdong JV inayofanya kazi ya kusambaza umeme vijijini wilayani Chato, – Nuhu Mringo ameahidi kuendelea kufanya kazi hiyo kwa kasi na kwa viwango.

Ikiwa wilayani Chato, Bodi hiyo ya REA pamoja na mambo mengine, imekagua kazi ya usambazaji umeme katika vijiji vya Mutundu, Kakindo, Kamanga, Mnekez, Kakeneno na Matofali.