Katibu Chongolo ataka ujenzi wa mabweni shule za msingi Longido

0
214

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameitaka serikali kuendelea kujenga mabweni katika wilaya ya Longido ikiwa ni mkakati wa kuiinua wilaya hiyo katika sekta ya elimu kutokana na umbali uliopo kati ya kijiji kimoja na kingine unaokadiriwa kuwa ni wastani wa kilometa 60 na uwepo wa wanyama wakali.

Chongolo ametoa maelekezo hayo katika ziara ya kikazi ya Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan mkoani Arusha.

Akifafanua maelekezo hayo, ameeleza kuwa, kuna shule ya msingi ipo kijiji cha Irichang’isapukini kata ya Gerairungwa wilayani Longido, iliyopo umbali wa kilometa 130 kutoka Makao Makuu ya Wilaya, imeshakamilika kujengwa na mabweni yameshajengwa, wananchi wanasubiri idhini kutoka serikalini ili iingizwe kwenye bajeti ya shule za bweni.

Katibu Mkuu Chongolo, ameitaka Serikali kuharakisha kuiingiza shule hiyo kwenye mpango wa bajeti wa shule za bweni, ili ianze kupokea wanafunzi wa bweni kama inavyofanyika katika shule za msingi za Sinya, Longido na Ketumbeine ambapo zote hizi zinahudumiwa na serikali kwa asilimia 100.