Karakana ya kisasa ya JWTZ yazinduliwa

0
181

Rais John Magufuli amesema kuwa karakana ya kisasa ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyoizindua, ni msaada mkubwa kwa jeshi hilo kwa kuwa itapunguza gharama za utengenezaji wa magari ya Jeshi.

Rais Magufuli ambaye pia ni Amiri Jeshi wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ametoa kauli hiyo wakati akizundua karakana kuu ya JWTZ iliyopo kikosi namba 501 Lugalo jijini Dar es salaam.

Amesema mbali na kupunguza gharama za utengenezaji wa magari ya Jeshi, pia itasaidia kutoa mafunzo ya ufundi na kuwaongezea uwezo wa kiufundi askari wa JWTZ.

Ameishukuru serikali ya Ujerumani kwa kufadhili ujenzi wa karakana hiyo ambayo kwa sasa ndio kubwa na ya kisasa kati ya zote zinazomilikiwa na JWTZ, pamoja na misaada mikubwa wanayoendelea kutoa kwa Tanzania katika sekta mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya serikali ya Ujerumani, Balozi wa nchi hiyo hapa nchini Regin Hens  amesema kuwa, Tanzania ni kituo muhimu cha amani duniani hivyo wataendelea kushirikiana nayo.

Karakana hiyo imejengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 8.5.