Kambi ya matibabu ya Moyo yazinduliwa JKCI

0
201

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amezindua kambi ya siku Nane ya matibabu ya Moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na kuishukuru Taasisi ya Sharja Charity International kwa kuwezesha upatikanaji wa Madaktari bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Falme za Kiarabu kushiriki kwenye kambi hiyo.

Kambi hiyo inayofanya upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya Moyo zaidi ya Arobaini, imeanza Septemba 13 na itafikia tamati Septemba 20 mwaka huu, ambapo Taasisi ya Islamic Foundation kwa kushirikiana na Ubalozi wa Falme za Kiarabu hapa nchini wametoa ufadhili wa kuwezesha matibabu hayo.

Akizindua kambi hiyo, Waziri Ummy Mwalimu ameushukuru Ubalozi wa Falme za Kiarabu kwa kusaidia upasuaji kwa watoto wenye matatizo ya Moyo wa hapa nchini na kueleza kuwa kambi kama hiyo pia inatoa nafasi kwa madaktari kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kupata uzoefu wa matibabu ya Moyo.

Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa, pamoja na jitihada hizo kutoka kwa Wafadhili, Serikali pia imetenga Shilingi Bilioni 1.2 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kukamilisha chumba cha Tatu cha upasuaji wa magonjwa ya Moyo katika Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya upasuaji.

Kwa upande wake Balozi wa Falme za kiarabu hapa nchini Khalifa Abdulrahman Al-Mazzooqi amesema kuwa, ubalozi huo utaendelea kusaidia jamii ya Kitanzania katika nyanja za Elimu, Afya pamoja na huduma kwa akina mama.

Amesema kuwa msaada huo wa kambi ya matibabu ya Moyo sio wa mwisho, na wataendelea kusaidia zaidi sekta ya afya kwa kuwezesha matibabu kwa Wagonjwa wa Moyo na magonjwa mengine.

Awali akitoa taarifa ya kambi hiyo ya Matibabu ya Moyo kwa Waziri wa Afya, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Profesa Mohamed Janabi amesema kuwa hii ni mara ya Tatu kwa Taasisi ya Islamic Foundation kushirikiana na Ubalozi wa Falme za Kiarabu kuendesha matibabu hayo ya Moyo hapa nchini na kwamba tangu kambi hiyo imeanza ni mgonjwa mmoja pekee ndiye aliyefariki Dunia kati ya wagonjwa 65 waliofanyiwa upasuaji huo.

Profesa Janabi ameushukuru Ubalozi wa Falme za Kiarabu kwa kuwezesha matibabu ya Moyo kwa Watanzania, kwani wengi wanashindwa kumudu gharama za upasuaji wa Moyo kutokana na gharama hizo kuwa kubwa.