Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kuchuguza chanzo cha kuchafuka kwa Mto Mara, Prof. Samweli Manyele amesema uchunguzi wa kimaabara umebaini kuwa chanzo kikuu cha kuchafuka wa mto huo ni kusambaa kwa tope la uozo wa viumbe-vifu lililotibuliwa na mvua kubwa ilionyesha kwa kipindi cha muda mfupi.
Prof. Manyele amesema hayo leo akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma na kuongeza kuwa sababu kubwa ya kuchafuka kwa Mto Mara imetokana na mrundikano wa kiwango kikubwa cha tope lililosababishwa na uozo wa viumbe (organic matter) kilichobainika chini ya ardhi oevu ya huo.
Amevitaja viumbe hivyo ni pamoja na mimea ya matete, magugu maji na uwepo wa vinyesi vya wanyama uliosababishwa na wingi wa mifugo iliyopo katika eneo hilo.
Vilevile, Kamati yake imebaini kukosekana kwa hewa ya Oksijeni katika maji ya Mto Mara hali iliyopelekea vifo vya Samaki nakusema kuwa hali hiyo imetokana na mmeng’enyo wa viumbe-vifu wakati wa uozeshwaji wake chini ya maji uliosababishwa na wingi wa mimea maji kwenye eneo oevu la Mto Mara.
Kufuatia kukamilika kwa taarifa ya kina ya uchunguzi wa kuchafuka kwa Mto Mara, Kamati ya Kitaifa imeshauri maji ya Mto huo yanaweza kutumika kwenye shughuli mbalimbali za binadamu kwa kuwa sampuli zilizochukuliwa na kufanyiwa vipimo hazikuonesha kuwepo kwa kemikali za sumu na kusema kuwa viumbe kama Samaki ni salama kwa matumizi ya binadamu.
“Samaki wa Mto Mara wanaweza kutumiwa kama kitoweo bila kusababisha madhara kwa afya ya binadamu,” alisisitiza Prof. Manyele.
Kuhusu maji ya Mto Mara kuwa meusi, Kamati imesema kuwa hali ya weusi wa maji utandelea kuwepo mpaka mvua zitakaponyesha kwa wingi na kusafisha mto huo.