Kaburi aliliandaliwa Mwalimu Nyerere kanisani

0
503

Yapo mengi unavyoweza kusimulia kwa namna unavyomfahamu Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa Tanzania aliyejijengea heshima kubwa ndani ya bara la Afrika na duniani kote wakati wa uhai wake na hata baada ya kufariki dunia.

Pamoja na mengi ya kusisimua yanayomuhusu Hayati Mwalimu Nyerere, acha tuangazie machache ambayo pengine hukuwahi kuyasikia ama umesika kwa juu juu tu.

Kwanza, Mwalimu Nyerere aliyefariki dunia Oktoba 14 mwaka 1999 huko London nchini Uingereza alizaliwa Aprili 13 mwaka 1922 kijijini Butiama Musoma, Mara katika familia ya kichifu.

Pamoja na kuzaliwa ndani ya familia ya kichifu, bado hakuacha kumcha Mwenyezi Mungu katika siku zote za uhai wake.

Na hili ndilo lililosababisha Mwalimu Nyerere kujengewa kaburi akiwa hai ndani ya kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria wa Damu ya Azizi ya Yesu jimbo la Musoma mkoani Mara, kanisa alilokuwa akiabudu mara zote awapo kijijini Butiama.

Kanisa hilo lenye historia kubwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lilijengwa mwaka 1990 na yeye mwenyewe kwa ufadhili wa shirika la Precious Blood la Roma, Italia huku ikielezwa kuwa vifaa vyote vya ujenzi wa kanisa hilo viliitoka nchini Italia.

Paroko Msaidizi wa kanisa hilo lenye uwezo wa kutumiwa na Waumini 300 kwa wakati mmoja Padre Philip Makondo anasema, ndani ya kanisa hilo kuna kaburi lililojengwa ili lije kutumika kwa ajili ya mazishi ya Mwalimu na lilijengwa mwenyewe akiwa hai na akiendelea kuwa muumini wa kanisa hilo.

“Tangu Kanisa hili likijengwa paliandaliwa sehemu maalum kukachimbwa kaburi ambalo lingetumika kumzika mtumishi wa Mungu Mwalimu Nyerere, alipokuja kusali alikuwa analiona kaburi hilo, lakini ikaja kuonekana yeye ni Rais wa Watanzania wote wenye dini na madhehebu mbalimbali na hivyo angezikwa kanisani kungeonesha yeye ni wa Wakatoliki pekee ndio maana akazikwa nyumbani kwake.” amefafanua Padri Makondo

Mpaka sasa katika kanisa hilo bado kuna viti viwili walivyokuwa wakitumia Mwalimu Nyerere na mke wake Maria Nyerere walipoenda kuabudu, na Mama Maria ameendelea kutumia kiti chake mara zote anapoenda kuabudu kanisani hapo akiwa kijijini Butiama.