Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam, imemuhukumu Mwandishi wa habari za uchunguzi Eric Kabendera kulipa faini ya Shilingi Milioni Mia Moja baada ya kukiri kosa la utakatishaji fedha.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Janeth Mtega ambaye pia ameamuru Kabendera kulipa faini ya Shilingi Laki Mbili na Nusu au kwenda jela miezi mitatu baada ya kukiri kosa la kukwepa kodi.
Na pia katika kosa hilo la kukwepa kodi, Kabendera ametakiwa kulipa fidia ya Shilingi Milioni 172.
Kabendera alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza agosti tano mwaka 2019 akikabiliwa na mashitaka matatu, ambapo amefutiwa shitaka moja la kuongoza genge la uhalifu.