Jukwaa la Wahiriri lakoshwa na mchakato wa kupata wagombea CCM

0
387

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepongeza uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuruhusu kurushwa moja kwa moja (live) kwenye vyombo vya habari, mikutano yake miwili, Mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM wa 2020.

Jukwaa hilo limeongeza kuwa limefarijika zaidi kwa waandishi wa habari kuruhusiwa kuwamo ndani ya ukumbi wa mkutano tangu mwanzo wa mkutano hadi ulipofungwa na kura kuhesabiwa huku vyombo vya habari vikishuhudia na kurusha matangazo hayo.

TEF imesema hatua hiyo imeongeza uwazi na kuziba mianya ya malalamiko na kuondoa uwezekano wa kutiliwa shaka uteuzi wa wagombea Urais wa chama hicho.

TEF imeshauri utaratibu huo wa CCM uhamie kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), mahakamani na bungeni, kwani mambo wanayojadili ni kwa maslahi ya taifa letu wa watu wake.

“Vyombo hivi vinapoanika ukweli kwa mtindo huu, hata wanaopinga au wenye nia na malengo ya kupotosha hushindwa kwa kuona aibu. Kimsingi, ukweli hufuta fitina,” imeeleza taarifa iliyotolwa na Deodatus Balile, Kaimu Mwenyekiti wa TEF.

Katika taarifa hiyo TEC imempongeza Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM kwa uamuzi huo na zaidi imempongeza Dk. Hussein Mwinyi kwa kuteuliwa kugombea Urais wa Zanzibar.