JPM: Tuendelee kumuomba Mungu atulinde na janga hili la Corona

0
505

Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 10 Aprili, 2020 ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki katika Parokia ya Mlimani, Wilaya ya Chato Mkoani Geita kusali Ibada ya Ijumaa Kuu iliyoongozwa na Padre Prof. Innocent Sanga kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Ibada ya Ijumaa Kuu huadhimishwa ikiwa ni kumbukumbu ya kusulubiwa na kufa kwa Bwana Yesu Kristo, zaidi ya miaka elfu 2 iliyopita.

Katika salamu zake, Rais Magufuli amemshukuru Padre Sanga kwa mahubiri yaliyowakumbusha Wakristo kuwa msalaba unaokoa, na kwamba kupitia msalaba Mungu ataiokoa dunia dhidi ya majanga mbalimbali ukiwemo ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).

Amebainisha kuwa kutokana na madhara ya ugonjwa huo duniani, upo uwezekano wa kutokea upungufu wa chakula, hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuzalisha chakula cha kutosha na pia amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi kila mahali walipo huku wakichukua tahadhari za kutoambukizwa kama wanavyoelekezwa na wataalamu.

Rais Magufuli amesisitiza kuwa Serikali imeamua kutowazuia watu ndani ya nyumba zao wala kufunga mipaka kwa kutambua madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na kufanya hivyo ndani ya nchi na kwa nchi 8 ambazo zinategemea kupata huduma na bidhaa kupitia Tanzania hususani Bandari ya Dar es Salaam.
Amewataka Watanzania wote kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili aiepushe dunia na janga la ugonjwa wa Corona.