JPM: Serikali haijazuia matumizi ya barakoa

0
187

Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo Februari 21, 2021 ameungana na waumini wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam kusali Misa Takatifu (Dominika ya kwanza ya Kwaresma).

Akizungumza na waumini hao Rais Magufuli amesema Wakristo ambao wapo katika kipindi cha Kwaresma na Waislamu ambao wanakaribia kuingia katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, waendelee kumuomba Mungu kwani pamoja na jitihada za kibinadamu za kukabiliana na ugonjwa wa Corona, Mungu ndiye muweza wa yote na husimama kwa kila jambo.

Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona kama zinavyoelekezwa na Wataalamu wa afya na kufafanua kuwa Serikali haijazuia matumizi ya barakoa katika kujikinga na kuambukizwa virusi vya Corona bali Watanzania wachukue tahadhari kwa kutumia barakoa zinazotengezwa hapa nchini zikiwemo za Bohari ya Dawa (MSD) au zinazotengenezwa na Watanzania wenyewe kwa kuwa barakoa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi zina mashaka kuwa si salama.

Aidha, Rais Magufuli amesisitiza kutumia njia za asili za kukabiliana na magonjwa ya kupumua ukiwemo ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kujifukiza (kupiga nyungu).

Amewataka Watanzania kuondoa hofu inayopandikizwa ambayo ina madhara zaidi, na amesisitiza kuendelea kumtumaini na kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kuwa njia za kujikinga kwa barakoa, kutogusana na kutokaribiana (social distancing) pamoja na kujifungia majumbani (lockdown) vimeonekana kutokuwa suluhisho la uhakika kwani mataifa yanayofanya hivyo watu wake wanapoteza maisha kwa maelfu ikilinganishwa na hapa Tanzania.

Rais Magufulia amempongeza Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Padre Dkt. Alister Makubi kwa mahubiri yaliyoeleza namna Yesu alivyojaribiwa na kwamba hata changamoto za sasa ikiwemo ugonjwa wa Corona ni majaribu ambayo yatapita.

Pia, amewashukuru Watanzania kupitia madhehebu yao ya dini mbalimbali kwa kuitikia wito wa maombi na kufunga ili Mungu atuepushe na maafa ya ugonjwa wa Corona unaosumbua dunia.