JPM na maisha ya siasa

0
299


 


 
Safari ya kisiasa ya Rais, Dkt. John Magufuli ilianza kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Biharamulo Magharibi ambayo sasa inaitwa Chato mwaka 1995, na mwaka huo huo aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Mzee Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi.

Nyota ya Rais Magufuli ilizidi kung’ara katika ulingo wa siasa ambapo mwaka 2000 alichaguliwa tena kuwa Mbunge wa Chato, na kuteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, nafasi aliyoishika hadi mwaka 2005.

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Rais wa wakati huo Jakaya Kikwete alimteua Dkt. Magufuli kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mwaka 2010, alirejeshwa tena katika Wizara ya Ujenzi na kufanya kazi kubwa ya kujenga barabara kadhaa nchini kote kwa kipindi kingine cha miaka mitano hadi mwaka 2015 ambapo aliamua kujitosa kuwania urais wa Tanzania.

Kazi ilikuwa kubwa ambapo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Magufuli aliwashinda wagombea wengine zaidi ya 40, na baadaye kuchaguliwa kuwa Rais wa Tano wa Tanzania.

Rais Magufuli alishinda pia nafasi hiyo kwa kipindi cha pili katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28 mwaka 2020.

Kipindi cha pili cha Urais wa Dkt Magufuli kilianza kwa kiapo cha Novemba 5 mwaka 2020, ikimaanisha kuwa amekaa madarakani kwa siku 132 pekee.