JPM akerwa na ucheweshwaji mradi wa machinjio ya Vingunguti

0
179

Rais John Magufuli ameelezea kusikitishwa na kitendo cha Watendaji wa mkoa wa Dar es salaam cha kuchelewesha mradi mkubwa wa machinjio ya mbuzi wa Vingunguti na kuahidi kufanya ziara ya kushtukiza katika machinjio hayo.

Akihutubia wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha Pipes Industries Company Limited jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amewaagiza Watendaji wote wa jiji la Dar es salaam kusimamia mradi huo ili ukamilike haraka.

Rais Magufuli amehoji kuchelewa kwa mradi wa ujenzi wa machinjio ya Vingunguti wakati serikali imekwishatoa Shilingi Bilioni 12.5 ili kukamilisha ujenzi huo.

Aidha Rais Magufuli amemuhoji Kaimu Meya wa Manispaa ya Ilala, -Omar Kumbilamoto kwanini mradi huo unachelewa ikiwa fedha zote zimekwishatolewa na serikali.

Baada ya kutoridhika na majibu hayo, Rais akawataka madiwani na viongozi wengine wa mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha wanasimamia miradi yote inayotekelezwa na serikali.