JPM aagiza kusimamishwa kazi Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Geita

0
219

Rais John Magufuli amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Geita, – Mhandisi Modest Apolinary kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za serikali.

Amemtaka Waziri Jafo kufanya hivyo haraka iwezekanavyo, ikiwa ni kazi yake ya kwanza mara baada ya kuapishwa hii leo.

Amesema hajafurahishwa na kitendo cha Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya Mji Geita kununua gari lenye thamani ya Shilingi Milioni 400 wakati wanafunzi hawana madawati.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo Ikulu Chamwino jijini Dodoma mara baada ya kuwaapisha Mawaziri 21 pamoja na Naibu Mawaziri 23.

Amemuagiza Waziri Jafo kufuatilia changamoto mbalimbali ndani ya Wizara yake ikiwa ni pamoja na matumizi mabaya ya fedha za serikali.

“Tamisemi kuna Challenge nyingi hasa katika matumizi mabaya ya fedha, Jafo umefanya vizuri sana lakini kwenye kudhibiti fedha bado na nilifikiria sana kukurudisha au kutokurudisha hapo, nataka niseme ukweli ili tuelewane, kwa hiyo hili la matumizi ni baya nataka kazi yako ya kwanza ni kwenda kumsimamisha Mkurugenzi wa Geita”, Rais Magufuli.