Jokate aja na kampeni ya kuhamisha Machinga

0
184

Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam imetambulisha kampeni ya kuwahamasisha wafanyabiashara wadogo kutoka katika maeneo yasiyo rasmi kwenda kwenye maeneo yaliyotengwa na Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutambulisha kampeni hiyo inayoitwa Temeke Gulio, Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo amesema itasaidia wananchi kupata bidhaa wanazohitaji kwa bei nafuu lakini pia wafanyabiashara kuuza bidhaa zao katika maeneo yaliyo rasmi kwa haraka zaidi tofauti na ilivyo kwa sasa.

“Kampeni Temeke Gulio ni sehemu ya kutoa elimu kwa wafanyabishara kuona umuhimu wa kufanya biashara zao kwenye maeneo rasmi ili kuondokana kero za mara kwa mara kwenye maeneo ambayo hayatambuliki,” amesema Jokate

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Elihuruma Mabelya amesema atasimamia fedha zilizotolewa na Serikali kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanafanya kazi kwenye maeneo rafiki.

Utambulisho wa kampeni hiyo umekwenda sambamba na ugawaji wa maeneo 20 kwa ajili ya wafanyabishara wadogo wa wilaya hiyo huku Serikali ikitoa zaidi shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule na maeneo rasmi ya kufanyia biashara kwa Machinga wilayani humo.