Jengo jipya la kisasa ambalo ni makao makuu ya benki ya CRDB lililozinduliwa mkoani Dar es Salaam na Rais Samia Suluhu Hassan mbali na kutoa huduma za kibenki litatumika kama makumbusho ya kufundishia.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela wakati wa uzinduzi wa jengo hilo.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Nsekela amesema benki ya CRDB yenye matawi zaidi ya 260 nchi nzima tayari imeanza kutoa huduma za kibenki nje ya nchi ambapo kwa sasa inatoa huduma hiyo nchini Burundi huku mipango ya kukamilisha maandalizi ya kufungua katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ikiendelea.
“Jengo hili lina vyumba 60 na linaweza kuhudumia wateja 200 kwa wakati mmoja huku tukiimarisha huduma zetu hasa katika mfumo wa kidigitali, haya yote tumefanikiwa kutokana na ushirikiano mzuri wa Serikali yetu na Wadau mbalimbali.” ameongeza Nsekela
Pia amesema benki ya CRDB imepunguza riba ya mikopo kwa akina Mama kutoka asilimia 24 hadi 14, huku wakiendelea kuwawezesha wajasiriamali kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata mafunzo ya kibiashara.